Get Paid To Promote, Get Paid To Popup, Get Paid Display Banner

Dar wahakikishiwa usalama Tamasha la Krisimasi

Posted by dani handrian
Na Samia Mussa.
 
IKIWA zimesalia siku 13 kufanyika kwa Tamasha la Kimataifa la Krisimasi, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Temeke limewahakikishia ulinzi wa uhakika Watanzania  wote watakaohudhuria tamasha hilo linalotarajia kuanza Desemba 25 katika uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam. 

Kutokana na hali halisi ya kuwa Watanzania wengi wamekuwa wakijitokeza katika matamasha ya kila mwaka yanayoandaliwa na Kampuni ya Msama Promotions, Dira ya Mtanzania lilitaka kujua kuhusiana na Jeshi la Polisi lilivyojipanga kuimarisha usalama siku ya Krimasi ambako Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo anasema kuwa kawaida Jeshi hilo limekuwa likijipanga vilivyo katika mikusanyiko ya namna hiyo hasa katika matamasha ya muziki wa Injili.

Kiondo anasema kuwa Jeshi la Polisi ni wajibu wake kuhakikisha hali ya usalama inapatikana katika kila mkusanyiko mkubwa wa watu hasa katika matamasha kama itakavyokuwa katika siku ya Krisimasi katika Uwanja wa Taifa. Anasema kuwa kawaida katika matukio makubwa kama Tamasha la Krismasi ambalo litakwenda kukusanya umati wa watanzanzia kwa nia ya kusikiliza neno la Mungu kupitia nyimbo za injili wataweka ulinzi wa hali ya juu kulingana na hali halisi ya kiusalama ilivyo ulimwenguni.

“Ni wajibu wetu kulinda usalama na kwamba tamasha linafanyika katika Uwanja wa Taifa, unawekwa ulinzi wa hali ya juu na wataalam wa mabomu pamoja na Mbwa wanakuwepo pale siku tatu kabla ya tamasha kwa ajili ya kufanya ukaguzi kila mahali eneo la uwanja,’’ anasema Kiondo.

Anasema mbali ya kufanya ukaguzi huo pia kuna  wingi wa maaskari watakao eneo kila upande kwa ajili ya kuimarisha ulinzi baada ya kujiridhisha na hali ya usalama wa kutokuwepo kwa hatari ya mabomu.
Kiondo anaeleza kuwa pamoja na kuwa hali si nzuri ya kiusalama kutokana na matishio ya ugaidi, Jeshi la polisi limejipanga vya kutosha ambapo alisisitiza kuwa wakazi wa Temeke na Watanzania kwa ujumla wasiwe na wasiwasi kwa kuwa hali ya usalama imeimarishwa hasa katika mikusanyiko.

“Katika kipindi cha Krisimasi tunalazimika kufanya kazi ya ziada, kutokana na hali ilivyo hivi sasa, tunapenda kuwahakikishia watanzania kwamba kila atakayekwenda kwenye Tamasha ajihakikishie kwamba yupo salama kabisa,” anasema Kiondo.

Anasema kila kamanda anawajibika katika eneo lake na endapo linatokea tatizo anawajibika moja kwa moja ikiwa ni pamoja na kuulizwa na rais Jakaya Kikwete kwamba alikuwa wapi wakati tatizo linatokea jambo ambalo Kiondo amesema halitatokea kwake ndio maana amejipanga vilivyo kuhakikisha hakuna hatari yoyote itakayotokea wakati wa Tamasha hilo la kimataifa.

Ni mara ya kwanza kufanyika kwa tamasha la Krismasi ambako kampuni ya Msama imekuwa ikiandaa pia Tamasha la Pasaka ikiwa ni miaka 13 sasa kwa nia ya kusaidia jamii ikiwa pamoja na kusomesha watoto waliopo katika mazingiza magumu katika ngazi ya shule ya msingi, Sekondari na Vyuo, vituo vya watoto wanaoishi katika mazingira magumu na wanawake wajane. 

Lengo la Tamasha hilo ni kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kisasa cha kutolea misaada (Center)  pamoja na kiwanda cha kisasa cha kuzalishia kazi za wasanii  kwa manufaa ya Taifa na watu wake, kwani kwa kufanya hivyo itakuwa imesaidia Watanzania wengi wenye ndoto ya kuwa wasanii wakubwa nchini.

Tamasha la Kimataifa la Krismasi linatarajia kuanzia kufanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Desemba 25, Morogoro Desemba 26, ambako pia linatarajia kuwafikia wakazi wa  Tanga Desemba 28, Arusha Desemba 29 na Dodoma  Januari 1 mwaka 2014.
 

Copyright © 2009 ikpopped | Design by [blogger merak dua]