AFISA masoko wa soko la hisa la Dar es salaam, DSE, Magabe Maasa, akisisitiza jambo alipokuwa anawasilisha mada ya Soko la kukuza ujasiriamali, katika mafunzo ya wajasiriamali mkoani Mtwara,yaliyoandaliwa na DSE na kuhudhuriwa na wajasiriamali 100 ambayo yalifanyika katika ukumbi wa mikutano wa kanisa la kiinjili la kithule mjini hapa KKKT.
WAJASIRIAMALI wa Mtwara wakifuatilia kwa makini mada zilizokuwa zikiwasilishwa katika katika mafunzo yaliyoandaliwa na DSE na kuhudhuriwa na wajasiriamali 100 ambayo yalifanyika katika ukumbi wa mikutano wa kanisa la kiinjili la kithule mjini hapa KKKT.
WAJASIRIAMALI na wafanyabiashara mkoani Mtwara, wamehimizwa kuchangamkia fursa ya kukuza mitaji inayotolewa na soko la hisa la Dar es salaam, DSE kupitia kitengo chake cha kukuza wajasiriamali na kujipatia mitaji itakayokuza na kuhimalisha biashara zao.
Wito huo umetolewa leo na kaimu katibu tawala wa mkoa wa Mtwara Thimithes Pangisa, alipokuwa anafungua mafunzo ya siku mbili yaliyofanyika katika ukumbi mikutano wa kanisa la KKKT mjini haa yaliyolenga kuwaelimisha wajasiriamali na wafanyabiashara juu ya huduma ya ukuzaji wa wajasiriamali inayoendeshwa na soko la hisa la DSM.
Pangisa alisema kuwa kumekuwa na kawaida kwa baadhi ya watu kutojitokeza kushiriki pale fursa mbalimbali zinapojitokeza na pale wenzao waliojitokeza wanapoanza kunufaika ndipo nao huleta lawama kuwa wamebaguliwa au hawakushirikishwa jambo ambalo alisema linapaswa kuacha mara moja.
"Ndugu zangu wajasiriamali hii ni fursa muhimu na adhimu kwenu ichangamkieni siku zote mmekuwa na changamoto ya ukosefu wa mitaji sasa DSE leo imekuleteeni elimu hii ili mujue ni namna gani mnaweza kunufaika kwa kujipatia mikopo na kukuza biashara zenu", alisema Pangisa.
Akimkaribisha mgeni rasimi kufungua mafunzo hayo afisa masoko wa DSE,Magabe Maasa, alisema kuwa mafunzo hayo ni mwendelezo wa kampeni ya kuelimisha wajasiriamali na umma kwa ujumla juu ya huduma za kitengo hicho kipya kinacholenga kuwwainua wajasiriamali wadogo na wakati kwa kuwawezesha kupata mitaji ya kukuza biashara zao.
Maasa alisema kuwa tayari mikoa zaidi ya kumi imeshafikiwa na huduma hiyo na itaendelea hadi mikoa yote nchini ambapo kila mkoa wajasiriamali 100 wanahusishwa katika mafunzo hayo, chini ya ufadhili wa taasisi ya kuendeleza huduma za fedha (Financial sector developing trust kwa kwa mikoani mafunzo hayo huratibiwa na TCCIA.
Akiwasilisha mada ya Utawala bora wa kampuni na kuzingatia sheria, meneja wa utafiti na maendeleo wa soko la hisa la Dar es salaam, Ibrahimu Mshindo, aliwashauri wajasiriamali walio na makampuni kuzifanya kampuni zao kuwa za umma ili waweze kuuza hisa na kuingia katika mpango wa kukuza mitaji na hivyo kupata fursa ya kujikomboa na changamoto ya ukosefu wa mitaji walionao hivi sasa.
Aidha washiriki wa mafunzo hayo wameliomba soko hilo kuweka utaratibu wa kutembelea mikoani mara kwa mara ili kutoa elimu kwa wajasiriamali waishio mikoani waweze kujua shughuli za soko hilo na kunufaika na huduma zinazotoleawa.